Header Ads

ad

ZAWADI 7 UNAZOWEZA KUMPA MPENZI WAKO CHRISTMASS HII


Wakati saa chache zikiwa zimesalia kabla ya kufika sikukuu ya Christmas, siku chache pia zimesalia kabla ya kufikia sikukuu ya mwaka mpya.

Katika kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa mwaka, watu wengi hasa wapenzi, ndugu jamaa na marafiki hupeana zawadi mbalimbali kwa lengo la kupongezana na kwa namna mbalimbali. Zawadi hizo huwa za aina mbalimbali na hutegemeana na uwezo wa kiuchumi wa yule anayetaka kutoa zawadi hiyo.

Je! Umeshajua utampa zawadi gani mpenzi wako katika Sikuu hii ya Chritsmas na Mwaka Mpya? Kama bado basi hujachelewa sana, kwani hapa chini tumeorodhesha aina 7 za zawadi inazoweza kutoa kipindi hiki. Lakini haimaanisha kwamba ni lazima utoe zawadi hizo tu, au utoe moja wapo ya zilizotajwa, badala yake unaweza kutoa kulingana na uwezo wako.

Mavazi
Kwanza, mnunulie mpenzi wa mavazi anayoyapenda kama zawadi katika kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka. Mavazi hapa yanamaanisha zaidi ya nguo, ambapo ni pamoja na pochi, saa, hereni, vito vingine vya thamani kama pete, mikufu, rangi na vitu vingine vya urembo kama mafuta n.k. Zawadi hizi zinaweza kuwa kwa wote, mwanaume na mwanamke. Kama unajua kitu kizuri ambapo mwenza wako anapenda kukivaa lakini amekuwa akishindwa kununua ama alikuwa nacho lakini kimekwisha, unaweza ukamnunulia na kuongeza tabasamu katika uso wake.

Kabla ya kwenda kununua mavazi hayo, hakikisha unajua ukubwa wa nguo ama unajua kitu anachokipendelea ili kuepuka kutumia gharama na bado unayemletea zawa asiifurahie.

Utambulisho
Wengi hudhani kuwa zawadi ni lazima kiwe kitu kinachoshikika, lakini wanasahau kuna zawadi za kusaikolojia ambazo zitamfanya mwenza wako ajisikie kuwa yupo mahali sahihi na anachokifanya ni sawa. Wasichana wengi wanapofikisha kuanzia umri wa miaka 23 hutaka kuwa na uhakika kwamba kwenye uhusiano walimo, hawapotezi muda bali ni uhusiano wenye macho na una muelekeo mzuri, hivyo ukimtambulisha unamuongezea imani.

Kutambulishwa hapa kunaweza pia kufanywa kwa mwanaume na sio lazima kabisa iwe kutambulishwa kwa wazazi wa mhusika, kwani huko kuna taratibu za kufuata. Utambulisho huu unaweza kuwa kwa ndugu wengine, jamaa na marafiki zao. Usiwe na uhusiano ambao hata ukiulizwa kama huyo ni mpenzi wake, unaogopa kusema ukweli. Kumbuka, unapomtambulisha mpenzi wako, unamfanya ajiamini kwamba yupo mwenyewe ndio sababu upo huru kufanya hivyo

Thamani za ndani
Meza ya mpenzi wako imechakaa? Au imepitwa na wakati? Vipi kuhusu ile runinga yake yenye kichogo? Huwa anaona hata aibu kuiweka sebuleni?

Katika sikukuu hizi, unaweza kuamua kumnunulia mwenza wako thamani mbalimbali za ndani ambazo zitamfanya kila mara anapotumia au kukiona kitu ulichokinunua akukumbuke. Katika kipengele hiki unaweza kununua meza, makochi/sofa, kitanda, viti vya kukalia, vitu vya jikoni, jiko n.k.

Kuna usemi ambao husema kuwa, sio lazima ufanye kitu kikubwa, lakini unaweza kufanya kidogo kwa upendo mkubwa na kikamfariji sana yule utakayemfanyia. Usiidharau zawadi unayoweza kutoa, kwani hata wahenga walisema kuwa, zawadi haichaguliwi.
Vitabu

Watu wengi wakishahitimu shule huwa hawapendi sana kusoma, lakini hii haimaanishi kuwa ni wote, wapo ambao hupenda kusoma hasa vitabu vinavyozidi kuwaongezea maarifa na ujuzi kuhusu masuala mbalimbali maishani.

Kama mpenzi wako ni mmoja wa watu hao unaweza kumnunulia vitabu vya kujisomea, au kama wewe unapenda kusoma lakini yeye hapendi, unaweza pia kumnunulia na ukamhimiza na kumtia moyo hadi ajifunze kujisomea. Kuna faida kubwa sana katika kusoma.
Mbali na vitabu vya kujisomea, huenda mwenza wako bado ni mwanafunzi katika chuo fulani, unaweza ukachukua jukumu la kumnunulia vitabu vitakavyomsaidia katika masomo yake. Pia, unaweza kumnunulia vifaa vingine vya shule, kwani hii itaonyesha kuwa unaunga mkono jitihada zake anazozifanya na kumfanya ajisikie kwamba hayupo mwenyewe.

Chakula
Najua hapa tayari wengi wamefikiri kununua chakula katika mgahawa fulani, au kuagiza pizza na burger kwa ajili ya wapenzi wao. Sawa, si vibaya, lakini, umefikiri kuhusu kuingia jikoni na kumpikia mwenza wako? Hasa kwa wanaume ambao mara nyingi sio wanaopika, kwanini usimwambie mkeo/mpenzi wako wa kike apumzike na kwamba wewe ndio utapika. Amini, hata kama hataonesha wazi furaha yake, lakini ndani kwa ndani atakuwa amefurahi.
Kama unaogopa labda ukipika chakula kama pilau itatoka kama ugali, basi wala usijaribu maana utamfanya hata akasirike zaidi. Unachoweza kufanya hapa ni kumpeleka sehemu nzuri anapoweza kula chakula anachokipenda yeye na nyote mkafurahi.
Lakini tutoe wito kidogo kwa wale watakaopikiwa chakula, hata kisipokuwa kizuri, basi badala ya kaunza kumshushua mwenzako, mpongeze, kwanza ameweza kuonyesha uthubutu, kisha unamuelekeza namna bora ya kupika ili wakati mwingine kiwe kizuri zaidi.

Muda
Wakati mwingine, zawadi ambayo mpenzi wako anataka ni muda wako wa kikaa nae pamoja. Huenda kwa mwaka mzima umekuwa ukipambana na hali yako na hukupata muda wa kutosha wa kukaa pamoja na mpenzi wako (kama hamjaoana) mkajadiliana mambo yanayowahusu.

Unaweza kuutumia wakati huu wa sikukuu ambapo wengi hawaendi kazini, mkakaa pamoja na kuweka mipango ya maisha yenu katika mwaka mpya unaoanza au kupima mafanikio ya mipango mliojiwekeea wakati mwaka 2017 unaanza.
Watu hesema kuwa, zawadi kubwa sana mtu anayoweza kukupa maishani ni muda wake. Akikupa muda wake inamaanisha kwamba amekuthamini na ameacha vingine vyote kwa ajili yako.

Mfanyie anachokipenda
Kama miongoni mwa vitu tulivyovitaja hapo juu hakunahata kimoja ambacho mpenzi wako anakipenda au ambacho wewe ungetamani kufanyia, unaweza kufikiri kile anachokipenda au unachotaka wewe ukamfanyika. Kikubwa cha kuzingatia hapa, hakikisha una uhakika na uanchotaka kukifanya, haitakuwa na maana utumie gharama kufanya kitu halafu unayemfanyia asifurahie.

Watu huwa na mapendeleo tofauti, hivyo mjue mwenza wako, fahamu anapendelea nini, na kisha mfanyie.

Wakati ukifikiri zawadi ya kumpa mwenza wako, Swahili Times tunakusihi zingatia kipato chako kwani kuna maisha baada ya sikukuu. Na maisha hayo yanayoanza upya Januari yanakuja na changamoto na majukumu mengi zaidi.
Tunawataki sikukuu njema za Christmas na Mwaka Mpya.

No comments:

Theme images by merrymoonmary. Powered by Blogger.