Header Ads

ad

LOWASSA AVUNJA UKIMYA, AWAKARIBISHA CHADEMA WALIOKATWA CCM


Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amewaita wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliokatwa katika ugombea wa nafasi mbalimbali kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wafurahie demokrasia.

Amesema Chadema na upinzani kwa ujumla kuna maisha mazuri ya kisiasa, uhuru wa fikra na demokrasia halisi ambapo amesoma na kusikia baadhi ya viongozi CCM wamekatwa katika kugombea au kutetea nafasi zao kwa sababu mbalimbali huku jina lake likiendelea kutajwa.

“Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere alisema ni wakati muafaka kwa Tanzania kuwa na mfumo wa vyama vingi, pamoja na kwamba maoni ya Watanzania wengi (wakati ule kupitia tume ya Nyalali) kutaka kuendelea na mfumo wa chama kimoja, uamuzi ule ulilenga kuwapa Watanzania demokrasia ya kuwa na uwanja mpana wa kufanya siasa.

“Mimi nimetumia fikra hizo za Mwalimu na hakika hivi sasa ninafurahia demokrasia halisi huku niliko, kwa wote waliokatwa na wanahisi wameonewa waondokane na unyonge wa fikra kudhani kuwa bila CCM hakuna maisha, waje huku tufanye siasa kwa manufaa ya wananchi wetu,” amesema Lowassa.

Pamoja na mambo mengine, Lowassa amewataka Chadema kuwapokea kwa mikono miwili na wanachama hao wapya.
“Wale wanaoendelea kubaki huko CCM tuendelee kushikamana hadi uchaguzi mkuu ujao 2020, tutakapoonesha makucha yetu, vitisho na nguvu ya dola inayotumika kujaribu kutunyamazisha sisi wa upinzani isiwatishe wala kuwaongofya hata mara moja,” amesema Lowassa.

No comments:

Theme images by merrymoonmary. Powered by Blogger.