Header Ads

ad

WATU WASIOJULIKANA WAWAUA WANANDOA WAKIWA WAMELALA


Wanandoa wawili Adam Charles Mtambo 41 na Mkewe Catalina Gabriel 39 wakazi wa Kitongoji cha Kasekese B Kata ya Kasekese Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi wameuawa kikatili kwa kukatwa na mapanga na kushambuliwa kwa silaha za jadi katika sehemu mbalimbali za mwili wao wakati wakiwa wamelala pamoja kwenye kitandani kwao.

Afisa Mtendaji wa Kata hiyo ya Kasekese Ramadhani Ibrahim alisema kuwa tukio hilo la mauaji hayo ya kikatili limetokea usiku wa kuamkia Jumamosi Oktoba 14,2017 majira ya saa saba kasorobo nyumbani kwa wanandoa hao.

Alisema marehemu Adam ambae alikuwa ni mfanya biashara anayemiliki maduka mawili Kijijini hapo, siku hiyo alifanya biashara ya kuuza duka kama ilivyo kawaida yake na baada ya muda wa kufunga duka ulipofika alifunga na waliingia ndani nyumba yao kulala yeye na mke wake.

Alieleza kuwa wakati wakiwa wamelala ndani walitokea wauaji hao ambao wanasadikiwa kuwa watatu na walifyatua risasi tatu za bunduki hewani na kisha walivunja mlango na kuingia ndani ya chumba moja kwa moja walichokuwa wamelala wanandoa hao.
Alisema baada ya kuingia chumbani waliwakuta wanandoa hao wamelala kitandani na ndipo walipoanza kuwashambulia kwa kuwakata kata kwa panga katika sehemu za usoni na kichwani na kuwashambulia kwa kutumia silaha za jadi ikiwemo marungu na fimbo.

Asifa Mtendaji huyo wa kata alieleza kuwa marehemu alijaribu kuwasihi waache kuwashambulia na aliwaeleza kuwa kama shida yao ni fedha basi waache kuwakata kwa mapanga na kuwashambulia kwa silaha za jadi na yeye yuko tayari kuwaonyesha mahali fedha zake zilipo ili wasiendelee kuwashambulia.
Pamoja na kuwasihi hivyo wauaji hao waliendelea kuwashambulia tu kwa mapanga hali ambayo iliwafanya marehemu na mkewe wazidi kupiga mayowe ya kuomba msaada kwa majirani wao .

Alisema kutokana na mayowe hayo watoto wa marehemu ambao nao walikuwa wakiishi kwenye nyumba hiyo wakiongozwa na kaka yao aitwaye Charles waliingia chumbani kwa wazazi wao kwa lengo la kutoa msaada.
Hata hivyo walishindwa kutoa msaada baada ya kushambuliwa na watu hao kwa kuwapiga na marungu na fimbo hali ambayo iliwafanya wakimbilie kwenye vyumba vyao vya kulala na kujifungia .

Majirani walifika kwenye eneo hilo na walikuta mlango wa mbele wa nyumba hiyo ukiwa umevunjwa na walipoingia kwenye chumba walichokuwa wanalala marehemu hao waliwakuta wakiwa wamelala chini ya kitanda huku wakiwa na majeraha makubwa katika sehemu mbalimbali za mwili wao huku damu zikiwa zimetapakaa kwenye chumba hicho .
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kasekese Happnes Bona alisema jitihada za kutafuta usafiri kwa ajili ya kuwafirisha wanandoa hao kwa ajili ya kuwapeleka katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda zilifanyika na hata hivyo wakati wakiwa njiani baada ya muda mfupi wanandoa hao walifariki.

Alisema tangu amekuwa Mwenyekiti wa Kitongoji hicho hajawahi kuona mauaji ya kutisha na y akikatili kiasi hicho kwani marehemu hao waliuawa kwa kukatwa katwa kama wanyama na sio kama binadamu .

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya Wilaya ya Mpanda na baada ya uchunguzi wa kidaktari.
Katika hali inayotajwa kuwa huenda vifo hivyo vimetokana na visasi,wauaji hao hawakuondoka na kitu chochote baada ya kutekeleza mauaji hayo.
Jeshi la polisi mkoani Katavi limethibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Na Walter Mguluchuma- Malunde1 blog Katavi

No comments:

Theme images by merrymoonmary. Powered by Blogger.