ORODHA YA MAMILIONEA 10 WAPYA WANAOTAMBA TANZANIA
Idadi ya mabilionea wa Tanzania kwa mujibu wa Jarida la Forbes inaendelea kuongezeka wakati taifa hilo liking’ara kiuchumi kulinganisha na mataifa mengine ya Afrika Mashariki.
Mbali na majina yaliyozoeleka ya mabilionea kama vile Mohamed Dewji, Rostam Aziz na Said Salim Bakhresa, kuna wengine wanaojulikana kidogo.
Majina hayo hayasikiki barani Afrika na kuna wanaofahamika kidogo hata ndani ya nchi, lakini ni wafanyabiashara waliofanikiwa nchini Tanzania.
Wafuatao kwa mujibu wa Forbes ni wafanyabiashara mamilionea 10 ambao wanamiliki biashara zinazoingiza kipato cha dola za Marekani milioni 50 au zaidi kwa mwaka.
Ally Awadh
Mfanyabiashara wa mafuta nchini Tanzania, Ally Edha Awadh ni mwasisi na Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Kampuni ya Lake Oil Group, moja ya himaya za kibiashara katika sekta ya mafuta na uchukuzi zinazokua kwa kasi Afrika Mashariki.
Awadh alianzisha kampuni hiyo mwaka 2006 akiwa na umri wa miaka 26, wakati alipopokea moja ya vibali adimu vinavyotafutwa zaidi kutoka serikali ya Tanzania kuingiza na kuuza bidhaa za petroli katika soko la ndani.
Shekhar Kanabar
Mfanyabiashara Shekhar Kanabar (35), ni CEO wa himaya ya Kampuni ya Synarge, yenye umri wa miaka 50 ikianzia kwa umiliki wa familia nchini Tanzania na imejikita mizizi katika sekta ya uzalishaji, uhuishaji wa betri na vipuri vya magari.
Baba wa Kanabar alianzisha biashara hiyo katika miaka ya 1960 zikijihusisha na nguo, lakini zimekua tangu hapo na kuhusisha kampuni mbalimbali zenye waajiriwa zaidi ya 150 na mapato ya mamilioni ya dola.
Subash Patel
Mwaka 1992, Subash Patel alianza kujihusisha na biashara ya mashine mbalimbali jijini Dar es Salaam. Katika kipindi cha miongo miwili, ameigeuza biashara hiyo katika Motisun Group, himaya ya kampuni tofauti 15 katika sekta za chuma, madini, plastiki, rangi,usindikaji wa vyakula na mali zisizohamishika. Ana hoteli za kitalii ikiwamo Sea Cliff Resort ya Zanzibar na Hotel White Sands Dar es Salaam.
Ghalib Said Mohamed
Milionea Ghalib Said Mohamed alianza kwa kufanya kazi katika biashara za baba yake katika kilimo cha korosho na biashara nyinginezo kwa ujumla.
Haikuchukua muda akaondoka na kuanzisha kampuni ya GSM Group, himaya ya kampuni inayojihusisha na biashara mbalimbali kama vile uchukuzi, lojistiki, vyombo vya habari, uzalishaji, mali zisizohamishika na huduma za kifedha na rejareja.
Fida Hussein Rashid
Mwaka 1973 Fida Hussein Rashid alianzisha Kampuni ya Africarries Group, mwasisi wa biashara ya magari mitumba nchini Tanzania. Africarries ikaondokea kuwa moja ya kampuni za kwanza Afrika Mashariki kuingiza magari ya Kijapan kama vile Toyota katika ukanda huo. Kampuni hiyo kwa sasa ni msambazaji muhimu wa magari ya Eicher na Golden Dragon.
Salim Turky
Salim Turky Mbunge wa Mpendae (CCM) ni mmoja wa wafanyabiashara waliofanikiwa zaidi Tanzania. Himaya yake ya kampuni za Turkys, ambayo aliianzisha katika miaka ya 1980 inajishughulisha katika uzalishaji wa saruji, hoteli, hospitali na huduma za mawasiliano.
Yongesh Manek
Manek alianzisha himaya ya kampuni za MAC nchini Tanzania katika miaka ya 1980. Biashara yake maarufu zaidi ni Benki ya Exim, moja ya benki kubwa tatu nchini Tanzania linapokuja suala la wingi wa wateja na mali. Pia ni mmiliki wa Kampuni ya Bima ya Heritage na Strategis, taasisi inayoongoza ya Afya nchini (HMO).
Abdulaziz Abood
Mwingine ni Mbunge wa Morogoro Mjini, Abdulaziz Abood (CCM), ambaye pia ni mwanasiasa na mwanzilishi wa Abood Group, himaya ya kibiashara inayojishighulisha na kila kitu kuanzia usafirishaji wa abiria, usambazaji wa petroli, vyombo vya habari hadi uwindaji wa kitalii.
Yusuf Manji
Manji alirithi kampuni ndogo ya biashara kutoka kwa wazazi wake na kuigeuza kuwa Quality Group, himaya ya kampuni zilizojikita katika utoaji wa huduma za kifedha, huduma za afya, usindikaji wa chakula na mali zisizohamishika. Manji pia ni mwenyekiti wa klabu ya Yanga, ambayo inatajwa kuwa klabu ya mpira wa miguu iliyofanikiwa zaidi Tanzania.
Haroon Zakaria
Murzah Oils, kampuni ambayo Haroon Zakaria aaliianzisha mwaka 1997 ni moja ya kampuni zinazoongoza Afrika mashariki kwa uzalishaji wa mafuta ya kula kutokana na mimea, siagi za mikate na margarine, manukato na sabuni za kufulia. Kampuni hiyo ina rekodi ya mapato ya dola za marekani milioni 100 kwa mwaka.
No comments: