MFANYABIASHARA ASHAMBULIWA KWA RISASI NA KUUAWA NA WATU WASIOJULIKANA
Mfanyabiashara mmoja katika Mji wa Lupa Tingatinga, Wilaya ya Chunya, mkoani Mbeya, ajulikanaye kwa jina Nestroy Kyando ameshambuliwa kwa risasi na kufariki papo hapo na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi ambao walifanikiwa kumuibia kiasi cha fedha shilingi milioni 4 na kukimbia nazo.
Kwa mujibu wa mashuhuda aliyekuwepo katika eneo la tukio, Ibrahim Khalid, alieleza kuwa tukio hilo lilitokea majira ya saa 3:15 usiku siku ya Jumamosi, Septemba 16 mwaka huu katika duka la bidhaa za jumla la mfanyabiashara huyo.
“Tulikuwa pamoja na marehemu dakika kumi kabla ya tukio na baadae aliamua kwenda nyumbani kwake wakati mimi nikiendelea na shughulli dukani kwangu. Akiwa nyumbani, kundi la watu lilimvamia na kumcharaza kwa mapanga huku wakimdai awape funguo za sanduku lake la kuhifadhia fedha. Aliwapa funguo ili kuyaokoa Maisha yake,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa mpaka sasa watu wane wamekamatwa na polisi huku wakiendelea kuhojiwa ili kukamilisha uchunguzi.
Mwenyekiti wa Chama Cha Wafanyabiashara Kata ya Lupa Tingatinga, Fredrick Kisucha, Amesema kuwa wamesikitishwa na tukio hilo na kuongeza kwamba hilo ndilo tukio la kwanza la ujambazi lililowahi kutokea katika eneo hilo.
“Tukio hili linaonekana kuwa limefanywa na watu wenye uzoefu mkubwa kwani limetokea muda ambao bado watu wengi walikuwa wakiendelea na shughuli zao za kawaida. Kwa hivyo inaonekana wazi kabisa kuwa watu hawa walijipanga kwa muda mrefu,” alisema Kisucha.
No comments: