Header Ads

ad

Maofisa wa TRA watumia saa sita kumhoji Askofu Kakobe


Dar es Salaam. Watumishi 12 kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) jana walitumia zaidi ya saa sita kumhoji Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe.

Mwandishi wetu ambaye alipiga kambi nje ya kanisa hilo lililopo Mwenge, Dar es Salaam kuanzia saa tano asubuhi, alishuhudia kuwasili kwa watumishi ambao mara baada ya kushuka katika magari na kutaka kuingia ndani, walizuiwa na wahudumu wa kanisa hilo kwa takribani dakika 15.

Baada ya kuingia ndani, watumishi hao walitoka saa 11:48 jioni kwa staili ya aina yake. Tofauti na walivyowasili kwa magari saba, wakati wa kuondoka walijibana katika magari mawili yaliyoingia ndani ya kanisa hilo kuwachukua, huku mengine yakiondoka tupu.
Tukio la idadi kubwa ya watumishi kuonekana katika kanisa hilo imekuja zikiwa zimepita siku tano tangu Kamishna wa TRA, Charles Kichere kueleza nia ya mamlaka hiyo kuanza mchakato wa kufuatilia ulipaji kodi wa Askofu Kakobe.

Kichere alisema uamuzi huo unatokana na kiongozi huyo wa kiroho kutokuwamo katika kumbukumbu za ulipaji kodi za mamlaka hiyo.

Alitoa kauli hiyo baada ya kusambaa kwa picha za video zikimuonyesha Askofu Kakobe akiwa katika mahubiri kwenye kanisa hilo, akisema kiwango cha fedha alichonacho si tu ni zaidi ya kile cha Serikali, bali pia anaweza kuwakopesha fedha hata mawaziri.
Kiongozi huyo wa kiroho alirejea kauli yake hiyo katika ibada ya Jumapili iliyopita, safari hii akibainisha kuwa ana fedha nyingi kuliko Serikali zote duniani na kuwataka watu wakimsikia anazungumza, watafakari kwanza kabla ya kumkabili.

Gazeti hili lilipotaka kupata ufafanuzi kwa Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo kama watumishi hao waliokuwa kwa Askofu Kakobe ni wa mamlaka hiyo, alishindwa kukubali au kukataa.

Alisema ingawa mamlaka hiyo iliahidi kwenda kumhoji hana uhakika kama hao walikuwa maofisa wa TRA au la.

Hata hivyo, mtendakazi wa kanisa hilo, Natus Mwita alipoulizwa kuhusu ujio wa maofisa hao alisema walipokea barua ya TRA tangu Desemba 30, mwaka jana.
Walileta barua yao kutaka kuonana na Askofu Desemba 30, sasa hatujajua labda leo wamekuja kuchukua mujibu yao, kwa sasa hamuwezi kuingia ndani labda msubiri nje ndiyo mtaweza kuonana nao watakapokuwa wakitoka,” alisema Mwita.

Jitihada za mwandishi wetu kuzungumza na watumishi hao ziligonga mwaba kutokana na kutotoka nje baada ya kumaliza mahojiano hayo kwani waliingia ndani ya magari hayo wakiwa ndani ya kanisa na kutoka katika mwendo wa kasi.

Wakati wakiwa ndani ya kanisa hilo, magari yenye namba za STK na STL yalikuwa yakipita mara kwa mara nje ya kanisa hilo lililopo kando ya Barabara ya Sam Nujoma.
Katikati ya mazungumzo hayo, Askofu Kakobe alitoka kwenye chumba cha mahojiano na kuelekea jengo jingine kanisani hapo. Baada ya kutoka baadhi ya watumishi hao wa TRA nao walitoka kwenye chumba hicho na kuonekana wakizungumza nje. Walirejea walirejea ndani baada ya askofu huyo kurudi.

Shughuli zaendelea
Wakati wote wa mahojiano hayo, shughuli mbalimbali za kanisa zilikuwa zilikuwa zikiendelea huku waumini wakionekana kuingia na kutoka.

Mmoja wa waumini hao, Janet Mathew alisema, “Nimekuja kwa ajili ya huduma ya maombezi na maombi kwa kweli hakuna shida yotote nimepata huduma vizuri.”
Alipoulizwa kama aliona tofauti yoyote na siku nyingine alisema, “Sijui kinachoendelea ni sawa na siku zote sijaona tofauti yoyote.”

No comments:

Theme images by merrymoonmary. Powered by Blogger.