Header Ads

ad

MASHTAKA MATANO ALIYOSOMEWA MKURUGENZI MTENDAJI WA AZAM MEDIA MAHAKAMANI


Mkurugenzi Mtendaji wa Azam Media Limited, Tido Mhando leo Januari 16 wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam na kusomewa mashtaka matano yanayomkabili na kisha kuachiwa kwa dhamana.

Tido Mhando ambaye alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) amesomewa mashtaka manne ya matumizi mabaya ya madaraka na moja la kuisababishia Serikali hasara ya Sh887 milioni akiwa TBC.
Tido alifikishwa mahakamani hapo saa 5:22 asubuhi na aliingizwa katika ukumbi wa mahakama ya wazi kabla ya kusomewa mashitaka hayo.

Akisoma mashtaka ya mtuhumiwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Makahama ya Kisutu, Victoria Nongwa, Wakili wa TAKUKURU, Leonard Swai ameiambia mahakama kuwa, Juni 16, 2008 akiwa Dubai, United Arab Emirates (UAE), Tido kama mwajiriwa wa TBC na Mkurugenzi Mkuu kwa makusudi alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mkataba wa makubaliano kwa ajili ya kuendesha na kutangaza vipindi vya runinga kati ya TBC na Channel 2 Group Corporation ( BV1) bila ya kupitisha zabuni, kinyume na sheria ya manunuzi na kuisababishia BVl kupata manufaa.

Shtaka la pili, Tido anadaiwa Juni 20, 2008 katika maeneo ya utekelezaji wa kazi yake alitumia madaraka vibaya kwa kusaini makubaliano (wakuu wa makubaliano) kwa utangazaji wa digital duniani kati ya TBC na BVl.

Shtaka la tatu, Agosti 11, 2008 na Septemba 2008 katika maeneo hayo, Tido anadaiwa kutumia vibaya madaraka yake kwa kusaini mkataba wa makubaliano (kuongeza wakuu wa mkataba ) kwa ununuzi, usambazaji kufunga vifaa vya usambazaji na mnara wa utangazaji kati ya TBC na BVI na kuisababishia BVI kupata faida.

Shtaka la nne, Tido anadaiwa Novemba 16,2008 akiwa Dubai, United Arab Emirates alitumia vibaya madaraka yake kwa kusaini mkataba wa makubaliano (kuongeza wakuu wa mkataba ) kwa kuendesha miundombinu ya utangazaji (DTT broadcast infrastructure) kati ya TBC na BVI na kusababisha BVI kupata manufaa.

Katika shtaka la tano, Tido anadaiwa kati ya Juni 16 na Novemba 16, 2008 katika maeneo hayo ya United Arab Emirates aliisababishia hasara TBC ya Sh 887, 122,219.19.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, mtuhumiwa alikanusha na akaachiwa baada ya kutimiza masharti ya dhamana. Kesi imeahirishwa hadi Februari 23, 2018 kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali (PH).

No comments:

Theme images by merrymoonmary. Powered by Blogger.