Tatizo la upungufu wa nguvu za kiume latinga bungeni, Mhe Kigwangalla atolea ufafanuzi
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imesema inatambua uwepo wa tatizo la upungufu wa nguvu za kiume hapa nchini.
Hayo yameelezwa na Naibu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe Dkt Khamis Kigwangalla wakati akijibu swali leo bungeni lililoulizwa na Mbunge wa jimbo la Konde, Mhe Khatib Haji swali lililohoji
Kumekuwa na ongezeko kubwa kwa tatizo la wanaume kupungukiwa nguvu za kiume Je, Serikali inajua tatizo hilo? na kama inajua inachukua hatua gani kukabiliana na tatizo hilo?
“Serikali inatambua uwepo wa tatizo hilo japo kuwa hakuna jibu la moja kwa moja la kufahamisha umma ukubwa wa tatizo hili kwa sababu tendo la ndoa ni tendo linalofanyia katika mazingira ya usiri kati ya wanandoa wenyewe“,amesema Mhe Kigwangalla huku akieleza sababu zinazosababisha tatizo hilo.
“Tatizo hili kwa kiasi kikubwa linawapata watu wenye umri mkubwa hasa kuanzia umri wa miaka 60 na wagonjwa wenye magonjwa sugu mbalimbali kama vile wenye shinikizo la damu, kisukari ,kifua kikuu, Kansa, ukimwi na wale wanaotumia dawa kwa muda mrefu, hata hivyo mwenendo wa tatizo hili kwa sasa hauzingati umri kuwa mkubwa linawapata watu wa rika zote, vijana na hata watu wazima kwa wazee tatizo la nguvu kupungua ni jambo la kawaida kwani kwa wanaume kadri umri unavyozidi kwenda tatizo hili linazidi kuongezeka uwezo wa kufanya tendo la ndoa unazidi kupungua taratibu pia husababishwa na ukosefu wa afya njema“,ameeleza Mhe Dkt Kigwangalla.