WABUNGE WAVUTANA MUDA WA RAIS KUKAA MADARAKANI
Mbunge wa Jimbo la Chemba, Juma Nkamia (CCM) pamoja na Mbunge wa Tarime Vijijini John Heche (CHADEMA), wamejipanga kwa nyakati tofauti kuwasilisha bungeni hoja binafsi kuhusu muda wa Rais kuwepo madarakani.
Wakati Nkamia akitaka muda wa Rais kukaa madarakani kongezwa kutoka miaka mitano mpaka kufikia saba, kwa upande wa Heche yeye anataka muda wa Rais kukaa madarakani upunguzwe kwa mwaka mmoja kutoka miaka mitano mpaka minne.
Hivi karibuni, Nkamia ameandika katika mtandao wa kijamii kwamba ameandaa hoja kuhusu suala hilo ambayo amejipanga kuiwasilisha bungeni.
Barua iliyotolewa na Bunge inaonyesha kuwa Mbunge Nkamia ameshaliarifu Bunge kuhusu azma yake.
Siku chache baadae Heche nae aliibuka na wazo tofauti akisema kuwa naye yuko mbioni kuwasilisha hoja binafsi kuhusu kupunguza muda wa Rais, wabunge na madiwani kukaa madarakani kuwa miaka minne.
Nkamia alieleza kuwa hoja yake inaungwa mkono na ukweli kwamba miaka mitano haitoshi kwa viongozi wa taifa kutekeleza mipango mikubwa. Alitoa mfano wa taifa la Rwanda ambapo muda wa rais kukaa madarakani ni miaka saba.
Kwa upande wa Heche, yeye alisema kuwa ni wakati wa Tanzania kufuata nyayo za taifa la Marekani ambalo Rais wake hukaa madarakani kwa kipindi cha miaka minne peke yake.
Wabunge wote hawa wamefanikiwa kuwapata wafuasi wanaounga mkono hoja zao na wapo ambao wanapingana nazo.
Makamu Mkuu wa Chuo cha Kikatoliki cha Ruaha, Prof. Gaudence Mpangala alisema kuwa amesikitishwa sana na hoja ya Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia, kwani huu siyo muda muafaka wa kuongeza kipindi cha uraisi.
No comments: