Header Ads

ad

FAMILIA YA LISSU YAFANYA KIKAO CHA SIRI NA UONGOZI WA BUNGE


Familia ya Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Tundu Lissu anayetibiwa hospitalini jijini Nairobi baada ya kushambuliwa kwa risasi septemba 7 mwaka huu, jana imefanya kikao cha siri na uongozi wa bunge kujadili matibabu ya Mbunge huyo.

Kikao hicho kimefanyika jana Jumatatu, oktoba 2, jijini Dar es Salaam na imeelezwa kuwa kilihudhuriwa na Spika Job Ndugai, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson, Katibu wa Bunge, Thomas Kashilila, Mbunge wa Vunjo, James Mbatia, Mbunge wa Hanang’, Dk Mary Nagu na ndugu watatu wa Lissu, wanaume wawili na mwanamke mmoja.

Kikao hicho kilianza asubuhi na kuisha majira ya saa saba mchana.
Mbunge wa Vunjo james Mbatia, baada ya kumaliza kikao hicho alikiri kuwa ni kweli kulikuwapo na kikao lakini hakuwa tayari kuzungumzia lolote kuhusiana na kikao na kuelekeza kuwa aulizwe Spika Ndugai.

“Ni kweli tulikuwa kwenye kikao na familia ya Lissu, lakini siwezi kusema tumezungumzia nini. Kwa taarifa zaidi nendeni kwa Spika au Katibu wa Bunge, walikuwepo pia ndugu zake watatu, wafuateni wanaweza kuwaeleza,” alisema Mbatia.

Msemaji wa familia ya Lissu, Alute Mughwai alisema kikao hicho kimefanyika kati ya familia na uongozi wa Bunge kuhusu mambo yanayomhusu Lissu, hata hivyo alisema hakijakamilika kwa sababu ya kukosekana kwa upande wa Chadema.

Mughwai alisema kikao hicho kimeahirishwa mpaka wakati mwingine pande zote zitakapotimia ili kulijadili suala hilo kwa ukamilifu wake. Alisema Chadema kupitia kwa mwenyekiti wake Freeman Mbowe walipewa mwaliko lakini hawakuweza kufika.

“Siwezi kukwambia tumezungumzia nini, moja ya masharti tuliyopeana ni kutokusema hadharani mambo tuliyoyajadili lakini yanamuhusu Lissu. Wote ‘interest’ yetu ni kuona Lissu anapona na kuendelea na majukumu yake kama kawaida,” alisema Mughwai.

Nae mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alipoulizwa kuhusu kikao hicho amesema taarifa kuhusu kikao hicho zilipelekwa Ofisi ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na siyo kwenye chama.

No comments:

Theme images by merrymoonmary. Powered by Blogger.