MAMBO YANAYOCHANGIA MTU KUWA MLEVI
Pombe na ulevi ni baadhi ya mambo yanayowasumbua watu wengi sana hapa nchini. Tabia hii ya matumizi ya pombe na ulevi umekuwa haichagui umri, siyo vijana, siyo wazee, wote wameingia katika mkumbo huu. Na wengi wao hawajui kuwa ina madhara, siyo tu kwa afya zao, bali pia katika familia zao na nchi kwa ujumla.
Ulevi umetajwa kuwa chanzo cha madhara mbali mbali yakiwemo kuvunjika kwa mahusiano, umasikini, ngono zembe, mimba zisizotarajiwa, ajali, maambukizi ya ukimwi na magonjwa ya ngono pamoja na mwengine mengi ya kufanana na hayo.
Vifuatavyo ni baadhi ya vitu vinavyoweza kukusababisha wewe kuwa mlevi.
Umri
Unapoanza kunywa pombe katika umri mdogo, unaongeza hatari ya wewe kuwa mlevi kwani utakapoizoea utafikia hatua kuiacha itakuwa ngumu sana.
Matatizo ya kisaikolojia
Watu wengi ambao wamekumbwa na matatizo ya kiakili, kifamilia au msiba na mengine kama hayo hujaribu kutumia vilevi kama njia ya kujisahaulisha matatizo yao. Ukweli ni kwamba pombe haiwezi kukusaidia kuyasahau matatizo, zaidi sana itakuongezea matatizo na hatari ya wewe kuwa mlevi.
Sababu za kimazingira
Kama marafiki zako na watu waliokuzunguka huwa wanakunywa pombe na ni walevi, basi hatari ya wewe kuingia katika wimbi la ulevi ni kubwa. Japo siyo lazima kutokea kwa jambo hili.
Historia ya familia
Hivi umewahi kusikia kuwa familia fulani ni ya walevi? kama hujawahi, basi zipo baadhi ya familia ambazo watu wake karibu wote ni walevi. Hii huchangiwa na wao kufuata nyayo za waliowatangulia. Kama babu alikuwa mlevi, utakuta watoto wake karibu wote ni walevi.
Mtaalamu wa baiolojia ya molekuli na mkurugenzi wa maabara wa Genemetric anasema kwamba baadhi ya watu huwa na jeni za ulevi na huzirithi kutoka kwa waliowatangulia. Hivi huwa katika mfumo wa neva.
Utu wako na namna unavyofanya maamuzi
Baadhi ya watu huwa hawawezi kufanya baadhi ya mambo pasipo kutumia vilevi au dawa za kulevya. Mfano, kuna wanaume hawawezi kuongea na msichana uso kwa uso kama hawajalewa, wapo wengine hawawezi kufanya baadhi ya mambo mpaka wawe wamekunywa pombe au dawa za kulevya. Kama una tabia hii, ukiiendekeza basi inaweza kukupelekea ukawa mlevi.
No comments: