Mashuti ya Ajib yampa kipa mke
STRAIKA Ibrahim Ajib wa Yanga mpaka sasa ana mabao mawili, lakini kama hujui ni kuwa straika huyo ndiye anayewanyima usingizi makipa wengi kwa kuwaliza sana uwanjani.
Lakini achana na hiyo, kipa wa zamani wa Yanga Benedictor Tinocco, aliyekaa Jangwani bila ya kudaka hata mechi moja, juzi alikuwa langoni wakati timu yake ya Mtibwa ikilazimisha suluhu na kupangua michomo mingi, huku akimtaja Ajib kama straika tishio nchini.
Tinocco alisema Ajib ni moja ya wachezaji wanamnyima raha uwanjani, lakini umahiri wake wa kuokoa mashuti ulimbeba na kufichua kazi hiyo ndiyo iliyompa mke aliyenaye kwa sasa.
Kipa huyo aliyeibuliwa na programu ya Taifa Stars maboresho, alisema uwezo wake wa kuokoa michomo ulimpa mke aitwaye Rozalina na kudai kabla ya mechi ya juzi alikuwa akimhofia Ajib.
“Ulikuwa ni mchezo wa kwanza msimu huu kwangu lakini niliingia nikijiamini, pia tulijipanga na kucheza kwa maelekezo ya makocha wetu, ila ukweli Ajib alikuwa akinyima raha ni mchezaji tishio nchini,” alisema.
Akizungumzia kiwango cha juu alichokionyesha alisema: “Unajua ni Mungu tu, pia kazi ile ya kuokoa michomo ni kazi yangu na ndiyo iliyonipa mke niliyenaye na nimezaa naye mtoto wa kiume, hivyo ni lazima niifanye kwa ubora.”
Rekodi za ubingwa
Juzi Yanga ilibanwa nyumbani na Mtibwa ikiwa ni mechi ya pili nyumbani kushindwa kutoka na ushindi msimu huu, lakini beki wake wa kati Andrew Vincent ‘Dante’ amefichua siri ya suluhu hiyo.
Yanga ilirudi Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam baada ya mechi tatu za ugenini Nyanda za Juu Kusini, tangu walipolazimishwa sare ya 1-1 na wageni wa Ligi Kuu msimu huu, Lipuli Iringa, lakini Mtibwa wakawabania tena. Dante alisema timu zinacheza kwa umakini ili kuepuka kuaibika mbele ya Yanga kutokana na rekodi ya kubeba ubingwa mara tatu mfululizo.
No comments: