Ngoma saa 48 chini ya uangalizi wa daktari
Mshambuliaji wa Yanga, Donaldo Ngoma atakuwa chini ya uangalizi wa daktari kwa saa 48 kuanzia leo Jumatatu, kutokana na maumivu ya msuli wa paja la mguu wa kushoto, aliyoyapata katika mchezo wao uliopita dhidi ya Mtibwa Sugar.
Ngoma alipata maumivu hayo kipindi cha pili cha mchezo wakati wanashambulia langoni mwa Mtibwa akashindwa kuendelea na mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Uhuru.
Daktari wa Yanga, Edward Bavu ameweka wazi maendeleo ya mchezaji huyo kupitia afisa habari, Dismas Ten aliyesema hali ya Ngoma inaendelea vizuri, lakini yuko kwenye uangalizi na hivyo hatafanya mazoezi ndani ya siku hizo mbili za uangalizi.
Ten alisema: "Daktari ameniambia, Ngoma anaendelea vizuri, lakini amepewa saa 48 kwa ajili ya uangalizi na vipimo vingine, ili kujua tatizo lake. Baada ya hapo ndipo itajulikana kama ataanza mazoezi au ataendelea na mapumziko pamoja na matibabu mengine."
Ten ameongeza kwa kusema, mshambuliaji huyo anaungana na Mrundi Amissi Tambwe anaendelea vizuri na anafanya mazoezi magumu ya pamoja na wenzake.
Kama hali itakuwa mbaya, huenda Ngoma akaukosa mchezo ujao wa Kanda ya Ziwa dhidi ya Kagera Sugar.
No comments: