RAIS MSTAAFU AWATAKA VIONGOZI WA SERIKALI KUTOJIUZULU
Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi amesema kuwa haoni sababu ya viongozi wa serikali kujiuzulu kutokana na mauaji yanayofanywa na watu wengine, badala yake mauaji ayo yakomeshwe ili kutooendelea kulifedhehesha taifa.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani ambayo huadhimishwa kila Oktoba Mosi, Mzee Mwinyi ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo alisema, hakuna haja kwa sasa kiongozi kujiuzulu kutokana na mauaji bali Serikali inapaswa kupambana na wauaji wote ili kutoruhusu hali hiyo kuendelea.
Mzee Mwinyi alisema kuwa, ni fedheha kubwa kwa taifa kwamba, sababu iliyomfanya ajiuzulu wakati akiwa waziri ambayo ni mauaji ya vikongwe, hadi leo bado yanaendelea kutokea.
Akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, mwaka 1976, Mzee Mwinyi alilazimika kujiuzulu nafasi yake baada ya kutokea mauaji katika Mkoa wa Shinyanga.
“”Hali ya kuongezeka kwa wazee ni jambo jema linaloonyesha Taifa linapata maendeleo lakini hili kuwaua vikongwe ni aibu na fedheha kubwa sana, naomba likomeshwe,” alisema Mwinyi
Aidha, Mzee Mwinyi amewashauri vijana katika maeneo mbalimbali nchini kujitolea na kuwatunza wazee katika maeneo yao ili kupata ushauri na busara za wazee hao kwa maendeleo yao na taifa kwani jukumu la kuwatunza wazee sio la serikali pekee.
“Niwaombe vijana mtutunze sisi wazee kwani na sisi tulikuwa vijana kama ninyi na mkiweka utamaduni huu utawasaidia na ninyi mkiwa wazee hapo baadae,”
alisema Mzee Mwinyi.
Pia, aliipongeza serikali kuwa, imejitaidi sana kuweka mazingira mazuri kwa wazee kwa kuwapatia huduma za Afya na kuwatunza wazee wote ambao hawana ndugu wa kuwatunza katika makambi mbalimbali ya wazee nchini.
Kwa upande wake Waziri wa Afya, MAendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amemuhakikishia Rais Mstaafu Mhe. Mwinyi kuwa Serikali itaendelea kuwatunza wazee nchini na kuhakikisha wanapata hudumu zote muhimu.
“Nikuhakikishie Mhe. Mwinyi kuwa tutaendelea kuwatunza wazee kwa kuwapatia huduma muhimu hasa huduma za Afya” alisema Waziri Ummy.
Naye Mwenyekiti wa Mtandao wa Wazee nchini Mzee Sebastian Bulegi amemuomba Mhe. Mwinyi kufikisha shukurani zao kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli kwa moyo wake wa kuwajali wazee nchini.
“Mhe. Mwinyi naomba utufikishie shukurani zetu kwa Mhe.Rais Magufuli kwa kutujali wazee hasa kwa kutatua changamoto zetu zinazotukabili” alisema Mzee Sebastian.
Siku ya Wazee Duniani huadhimishwa Oktoba Mosi kila mwaka kufuatia Azimio la Umoja wa Mataifa (UN) linalozitaka nchi wanachama kutenga siku maalumu ya kutafakari mchango wa Wazee katika maendeleo ya jamii na kuwaenzi ili wawe na maisha bora na yenye matumaini.
Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Mwaka huu ni “Kuelekea Uchumi wa Viwanda: Tuthamini Mchango, Uzoefu na Ushiriki wa Wazee kwa maendeleo ya Taifa”.
No comments: