Mbaroni kumgeuza mwanafunzi mkewe
MWALIMU mmoja wa Shule ya Msingi Samazi iliyoko wilayani Kalambo mkoani Rukwa, anashikiliwa na polisi mkoani hapa akituhumiwa kumbaka na kisha kumpa ujauzito mwanafunzi wa darasa la sita, mwenye umri wa miaka 15.
Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Judith Binyura, alisema jana kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa juzi baada ya mwanafunzi huyo (jina linahifadhiwa) kumtaja kwamba ndiye aliyempa ujauzito huo.
"Tumekuwa na utaratibu kuwapima watoto wa shule, ili kubaini kama wana ujauzito... sasa safari hii katika shule ya Samazi imegundulika mwanafunzi wa darasa la sita amepewa ujauzito na mwalimu wake," alisema mkuu huyo wa wilaya.
Jina la mwalimu huyo linahifadhiwa pia baada ya jitihada za kumtafuta kwa njia ya simu kupata kauli yake kushindikana jana.
Mratibu Elimu Kata ya Samazi, Daudi Sengo, alisema mwalimu huyo alikuwa akimtuma mwanafunzi huyo kufanya kazi za nyumbani kwake kama kufua, kusafisha nyumba na kumpikia chakula cha jioni; kisha kufanya naye mapenzi mara kwa mara.
Alisema awali ilikuwa vigumu kuthibitika kuhusu uhusiano wao wa kimapenzi hadi mwanafunzi huyo alipopimwa na kubainika ni mjamzito na alipobanwa na wazazi wake, alisema amepewa na mwalimu huyo.
Binyura alisema kuna tabia ya baadhi ya walimu kufanya mapenzi na wanafunzi wao, jambo ambalo halikubaliki kwa kuwa linawaharibu watoto hao kisaikolojia.
Alionya kwamba hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wale wenye nia mbaya na watoto wa kike waliopo masomoni.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa, George Kyando alikiri kwamba polisi inamshikilia mwalimu huyo na atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika, ili sheria ichukue mkondo wake.
No comments: