Header Ads

ad

SAKATI LA MADIWANI ARUSHA, TAKUKURU YAMGEUZIA ‘KIBANO’ MBUNGE NASSARI


Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imemtaka Mbunge wa Arumeru Mashariki (CHADEMA), Joshua Nassari pamoja na wabunge wangine wa chama hicho kuacha mara moja tabia ya kushinikiza taasisi hiyo kufanya kazi zake.

TAKUKURU imesema kuwa yenyewe ni taasisi huru ambayo haiwezi kushinikizwa na mtu yeyote na kwamba inafanya kazi zake kwa matakwa ya kisheria.
Hayo yamesemwa leo Oktoba 17 na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Valentino Mlowola, wakati akizungumza na waandishi kuhusu ushahidi uliopelekwa kwao na Nassari akidai kuwa Madiwani wa CHADEMA Arusha walinunuliwa na si kweli kwamba walijiuzulu kwa hiari yao kama ambavyo walieleza.

Mlowala amemtaka Nassari kuacha kuingiza siasa kwenye suala hilo la kisheria na kwamba, kwa sababu ameshafikisha madai yake katika mamlaka husika, awaache wafanye kazi yao ya uchunguzi.

“ Ni kama Mh. Nassari na wenzie wanataka kulifanya hili suala kama la kisiasa badala ya kuwa la kisheria. Kwa hiyo, namuonya Mh. Nassari, ameshaleta taarifa yake kwetu, atuachie tufanye yale yanayotupasa kufanya kwa mujibu wa sheria na sio kutushinikiza,” amesema Mlowola.
Kiongozi huyo ameonya zaidi kuwa, endapo Nassari ataendelea kuishinikiza taasisi hiyo kufanya kazi zake, watamchukulia hatua za kisheria bila kuathiri nafasi ya taarifa ambazo amewapatia na wanazoendelea kuzifanyia kazi.

Mlowola ametoa rai kwa wananchi wanaotaka kupelekea taarifa kwao kwamba, mara baada ya kuwasilisha taarifa zao, wakiache chombo chenye mamlaka kifanye kazi zake na sio kutaka kukiingiza katika ulingo wa kisiasa.
Akizungumzia hatua ya uchunguzi wa madai ya Nassari, Mlowola masema kuwa, mchakato wa kiuchunguzi ni wa siri wakati mwingine na kwamba matokeo yake yatadhihirika mahakamani.

“Katika taarifa ya jana walikuwa wanasema kwanini hatufiki mahakamani haraka. Nataka wafahamu kwamba, tunaongozwa na Sheria ya Mwenendo wa Mashtaka ya Jinai.”
Alisema kwamba, watakapomaliza uchunguzi, watatathmini ushahidi wao, na endapo utakidhi vigezo vinavyotakiwa na sheria, ambapo watapeleka jalada kwa Mwendesha Mastaka Mkuu wa Serikali (DPP) ambapo yeye ataandaa mashtaka dhidi ya watuhumiwa hao kulingana na ushahidi wao.

Aidha, alisisitiza kwamba, uchunguzi utakapokamilika ndipo watajua kama kilichofanyika ni kosa au sio kosa huku akifafanua kwamba, baadhi wanaweza wakadhani jambo fulani ni la jinai kumbe ni makosa ya kimaadili ambayo yana njia nyingine tofauti ya kushughulika nayo.
“Tunapokea taarifa, tunazifanyia kazi, lakini hatuwezi kukubali kuwa ‘dragged into politics’ (kuingizwa katika siasa),” alisema Mlowola.

No comments:

Theme images by merrymoonmary. Powered by Blogger.