UTEUZI ALIOUFANYA RAIS MAGUFULI WAIBUA UTATA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tazanania, jana alitangaza mabadiliko katika baraza la mawaziri ambayo yalihusisha kuongezeka kwa wizara kutoka 19 na hadi kufikia 21.
Vile vile alitangaza kumteua Steven Kagaigai kuwa Katibu mpya wa Bunge akiichukua nafasi ya katibu aliyekuwepo Dk Thomas Kashililla na kueleza kuwa atapangiwa nafasi nyingine.
Uteuzi huu wa Katibu wa Bunge uliofanywa na Rais Magufuli umezua mjadala na kuwashtua wakosoaji ambao wamedai kuwa kanuni, taratibu na sheria zimekiukwa.
Akizungumzia suala hili la uteuzi wa Katibu wa Bunge, Mbunge wa Kigoma Mjini kwa tiketi ya chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, alieleza kuwa Rais amekiuka sheria zinazopaswa kufuatwa ili kuteua Katibu.
Zitto alisema kwamba Sheria ya Utawala wa Bunge inamtaka Rais kuteua Katibu wa Bunge kutoka kwenye orodha ya watu watatu ambao wamependekezwa na Tume ya Huduma za Bunge. Lakini Rais Magufuli hakufuata utaratibu huo jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa Bunge limedhibitiwa.
Naye Mbunge wa Kaliua kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Mgdalena Sakaya ameeleza kuwa anashangazwa na uteuzi huo kwa sababu hakuna na kikao cha kupendekeza majina matatu kwa Rais ili afanye uteuzi kilichofanyika kama kanuni zinavyotaka.
Alisema yeye ni kamishna wa Tume ya Bunge ambayo hupendekeza majina hayo, lakini hajasikia kikao, tetesi, wala kufahamishwa kwa namna yoyote ile kama kuna uteuzi wa aina hiyo.
“Sijui kwa kweli nimesikia suala hilo kutoka kwako. Uwih!! Umefanyika uteuzi, kwa kweli hatujakaa na wala sijasikia,” alisema Sakaya.
Hata hivyo, Rais Magufuli alieleza kuwa mawaziri wote pamoja na manaibu wao walioteuliwa kama wataridhia uteuzi huo, zoezi la kuwaapisha litafanyika Jumatatu, Oktoba 9, 2017 ikulu Jijini Dar es Salaam.
No comments: