FAHAMU WALICHOZUNGUMZA LOWASSA NA NYALANDU BAADA YA KUKUTANA
Aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu ambaye hivi karibuni alitangaza kukihama Chama cha Mapinduzi (CCM), jana alikutana na kufanya mazungumzo na Edward Lowassa ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Nyalandu alifanya mazungumzo na Lowassa ambaye amewahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania katika serikali ya awamu ya nne kabla ya kutimkia chama kikuu cha upinzani mwaka 2015 wakati wa uchaguzi mkuu.
Akieleza walichojadiliana, Nyalandu kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii ameandika, “…nimekutana na kufanya mazungumzo na Mh. Edward Lowassa ofisini kwake, Mikocheni, mjini Dar es Salaam kuhusu umuhimu wa kuimarisha umoja miongoni vyama vya upinzani nchini Tanzania tukiwa tunaelekea Uchaguzi Mkuu 2020.”
Kama ilivyokuwa kwa Nyalandu, Lowassa alipohama CCM alisema kuwa miongoni mwa sababu zilizomsukuma kufanya hivyo ni madai ya chama hicho kupoteza mwelekeo na kutoridhishwa na mwenendo wake hasa namna ya ufanyaji maamuzi.
Licha ya kuwa hajatangaza rasmi kujiunga CHADEMA, wakati akitangaza kujiuzulu, Nyalandu alisema kuwa anawaomba kama itawapendeza wamruhusu kujiunga nao ili kuungana na CHADEMA na watanzania wote wanaopenda kuleta mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi nchini kwa kupitia mfumo wa ki demokrasia na uhuru wa mawazo.
No comments: