Header Ads

ad

Mitando ya kijamii inavyoipiku mikutano ya hadhara ya siasa


Hakika zama za kuandaa jukwaa, kualika wanachama, wanamuziki, washereheshaji na kusambaza vipeperushi kwa ajili ya kutangaza mkutano wa kisiasa, zinakufa.

Zama hizo zinauawa na silaha moja ndogo tu; mitandao ya kijamii. Hivi sasa mitandao ya kijamii ndiyo imegeuka majukwaa ya wanasiasa wanapotaka kueleza chochote wanachotaka kuueleza umma.

Iwe ni kutangaza nia, kung’atuka, kumjibu mshindani, kutoa ushauri au kuzungumzia mada yoyote ile ya kisiasa. Haya yote yanaweza kuwekwa katika ukurasa wa Twitter, Facebook, Instagram au hata chaneli ya video ya Toutube.

Rais John Magufuli, kama walivyo wanasiasa wengi, naye ni mtumiaji wa Twitter. Mara kadhaa anautumia kutoa pole, pongezi, shukrani au hata kueleza kuhusu kazi anayotarajia kufanya au aliyofanya au ziara zake za kikazi. Kwa mfano, Septemba 7, siku ambayo mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alipigwa risasi, Rais Magufuli aliandika alituma pole katika akaunti yake ya Twitter.

“Nimepokea kwa masikitiko tukio la kupigwa risasi Mh. Tundu Lissu, namuombea kwa Mwenyezi Mungu aweze kupona haraka,” unaeleza ujumbe huo.
Na hata baada ya aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini, (CCM) Lazaro Nyalandu kujiuzulu, wanasiasa wengi, wa chama tawala na upinzani walizungumza kupitia mitandao ya kijamii.

Kwa mfano, katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, aliyeeleea kuwa uamuzi huo ni demokrasia.
“Ibara ya 20 inatoa uhuru kwa mtu kujiunga na chama chochote na kuondoka kwa hiari. Hii ndio demokrasia,” anasema Polepole.

Kupitia Twitter, Nyalandu alitoa taarifa au kujibu tuhuma dhidi yake.
“Nawashukuru Watanzania wote walioniletea salamu kuunga mkono uamuzi wangu wa kujiondoa CCM. Turuhusu ushindani wa demokrasia ya kweli Tanzania,” aliandika
Inaendelea uk 26
Inatoka uk 25

Mtumiaji mwingine mzuri wa mitandao ya kijamii ni mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye a,naye hutumia njia hiyo kushauri ama kutoa ujumbe tata.

“Acheni kupiga ramli juu ya kesho yangu! Kisa mnatafuta vyeo na hamuwezi kutumia akili kufikiri! Sina press conference kesho,” aliandika Oktoba 30, akizungumzia taarifa zilizoenea kuwa aliitisha mkutano wa waandishi wa habari.

Oktoba 28 akaandika katika ukurasa wake akisema; “Mwenyezi Mungu akikupa ndoto anakupa na nguvu ya kuifanya ndoto itokee” Ujumbe huo uliambatanishwa na picha yake kwenye jukwaa akihutubia ndani ya sare za CCM.

Nape anaamini kwamba mitandao ya kijamii inawafikia watu wengi zaidi kwa sasa kuliko hata ilivyo kwa magazeti.
Kama gazeti la Mwananchi ambalo ndilo lenye wasomaji wengi zaidi, linachapisha kopi kwa mfano 70, 000 halafu asilimia 60 ya magazeti yakarudishwa (returns). Hivyo magazeti yanayowafikia watu pengine ni 40,000. Wakati huo, mimi nina wafuasi karibu 200,000, kwa kifupi nawafikia wengi kwa wakati mmoja, na kokote mtu aliko bila kutoa hela yake,” anasema

Anasema mitandao hiyo inawafikia watu ambao kila mmoja anaupokea ujumbe kwa namna tofauti na hilo linamwezesha kila mmoja kuonyesha hisia zake kwa wakati huo. Anasema jambo hilo limeleta mapinduzi makubwa.

Nape ambaye alikuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM; katika uchaguzi wa mwaka 2015 walitumia nyenzo hiyo hata kubashiri kiasi gani mgombea wao, anaungwa kwa mkono.
“Tuliwekeza kwa kiasi kikubwa, tuliweza hata kuhesabu kura zetu kupitia mitandao ya kijamii, unaweza ukapata picha ni kwa kiasi gani mgombea wenu anaungwa mkono, kwa mfano unaweza ukaweka katika mtandao, wangapi wanamuunga mkono Magufuli, utapata mrejesho, utajua ni kiasi gani anaungwa mkono,” anasema.

Anasema mitandao iliwasaidia kujua ni hoja zipo walizonazo wananchi; “Kwa mfano ukiweka katika mtandao kuwa kesho Magufuli atakuwa Mbeya, basi watakuambia hapa Mbeya kuna ABC, kwa hiyo mnamuandaa mgombea wenu kujibu hoja hizo.”

Mtumiaji mwingine mzuri wa mitandao ni mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa. Novemba 2 aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kuhusu hoja yake ya kumng’oa spika wa Junge, Job Ndugai.

“Hoja ya kumng’oa Spika iko palepale! Naamini wabunge wenye akili wataiunga mkono.”
Msigwa anasema mitandao haiepukiki. Anasema ili kuendana na kasi katika nyakati hizi mwanasiasa hana budi kutumia mitandao ya kijamii kuwafikia watu wengi kwa wakati mmoja.

Hata hivyo, Msigwa anasema bado majukwaa yana umuhimu mkubwa kwa wanasiasa kunadi sera zao.
“Unapozungumza nao (wananchi) uso kwa uso, unaleta ukaribu, ukaribu ambao wapiga kura wanautumia kuuliza maswali, kueleza hisia zao. Lakini pia, tukumbuke si wote wenye simu za mkononi,” anasema.

Mitando hiyo hutumika pia kueleza hisia kuhusu siasa za nje ya nchi. Kwa mfano, Novemba 15, Msigwa aliandika hivi katika ukurasa wake wa Twitter: `Zim is far bigger than Mugabe (Zimbabwe) ni kubwa zaidi kuliko (Robert) Mugabe, jeshi limefanya jambo jema kabisa, mtu hawezi kugeuza nchi kama mali yake. Majeshi Afrika yasitumike kulinda watawala wa aina ya Mugabe! Hii ni aina mpya ya mapinduzi.”

Watu 714 hadi juzi walibonyeza alama ya kupenda kauli hiyo, wafuasi wake 71 walisambaza kauli hiyo kupitia akaunti zao na wengine 47 walichangia mjadala huo kwa kuandika hoja zao.

Wanasiasa wengine wanatumia mitandao hiyo kueleza wanachofanya au walichofanya, ilimradi ule umuhimu mkubwa wa kufanya mkutano na kuwaita waandishi wa habari na wananchi kuwaeleza mipango ya miaka mitano ya maendeleo, ujenzi wa visima, miswada au hata maamuzi yaliyofanywa na Serikali sasa umepungua.

Si Tanzania tu, bali hata nje ya nchi ndivyo wanasiasa wanavyofanya. Mathalan, Rais wa Marekani, Donald Trump anaweza kutajwa kama bingwa wa kutumia Twitter kutoa hoja zake mbalimbali.

Kwa Afrika na Afrika Mashariki, mfano mzuri wa watumiaji wa Twitter ni Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ambaye mara kwa mara hueleza yale anayofanya kwa kupitia ukurasa wake wa twitter, kwa mfano hivi karibuni wakati alipokutana Mtukufu, Sheikh Mohammed Bin Zayed Al Nahyan, Mfalme wa Abu Dhabi, aliandika katika ukurasa wake: “Tumejadili tunayoweza kushirikiana baina ya nchi zetu katika maendeleo ya miundombinu, biashara, mafuta, gesi na nishati.”``

Ni kawaida kwa mwanasiasa kumlaumu mwandishi wa habari, pale ambapo habari yake iwe katika redio au katika gazeti haijatoka kwa urefu anaoutaka (kwa mfano kazungumza kwa dakika 30 lakini sauti yake inasikika kwa dakika 5 au anapata aya nne tu kwenye gazeti.
Lakini leo hii, mwanasiasa anaweza kujirekodi, au kuandika kwa urefu ujumbe anaoutaka na kusambaza kwa mashabiki wake, milioni moja au zaidi. Hiyo inampa muda usiochujwa wa kusema hoja yake.

Nape ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, amezungumzia wajibu wa vyombo vya habari katika mapinduzi haya ya wanasiasa kutumia mitandao ya kijamii kuliko majukwaa.

“Haina maana kama nitaisikia au nitasoma katika gazeti, habari ambayo kutwa nzima ya leo, nimeisoma katika mitandao ya kijamii. Siku hizi hata ajali imetokea sasa hivi, na wakati huohuo unapata taarifa kamili, idadi ya majeruhi na vifo,” anasema
Anasema kama chombo cha habari kitaishia palepale au kuripoti kilekile kilichoandikwa katika mitandao ya kijamii, kitakosa maana na uhalisia.

“Ni lazima kitafute habari nyingine zaidi au aende mbali zaidi, vinginevyo habari hiyo itakosa ladha na itakuwa hamna maana ya kuzingatia vyombo vikuu vya habari, ambavyo ni magazeti, runinga na redio,” anasema.

Nguvu ya mitandao ya kijamii ilionekana hata wakati Lissu alipopigwa risasi, Dodoma. Kwa kiasi kikubwa taarifa kuhusu kujeruhiwa kwake, kusafirishwa, na maendeleo yake baada ya kufika Hospitali ya Nairobi, yote yalichapishwa katika mitandao ya kijamii.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na mchungaji Msigwa, kila mara walitoa taarifa kupitia akaunti zao za mitandao ya kijamii kuhusu maendeleo ya Lissu.

Haikuishia hapo, hata Lissu alipopata nafuu na kuzungumza, alirekodi sauti na kusambazwa katika mitandao ya kijamii, akiwashukuru Watanzania kwa kuwa pamoja naye katika kipindi hicho.

Mzozo wa Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Nyalandu, na Waziri wa sasa, Hamis Kigwangalla, kwa kiasi kikubwa umechapishwa na kuendelea kukua kupitia katika akaunti zao za Twitter.

Baada ya Nyalandu kuhama CCM; Kigwangala alianza kutoa tuhuma mbalimbali dhidi ya Nyalandu. Lakini mbunge huyo wa zamani wa Singida Mashariki naye alijibu tuhuma hizo kupitia mitandao hiyohiyo. Kwa kifupi hakukuwa na haja ya jukwaa kati ya mahasimu hao wawili.

Majibizano haya katika mtandao wa twitter, yalimuhusisha pia Waziri mwingine wa zamani wa wizara hiyo, Balozi Hamis Kagasheki ambaye pia ni mtumiaji mkubwa wa twitter.
Mtaalamu wa mitandao ya kijamii, Job Simalenga kutoka Chuo Kikuu cha Daystar, nchini Kenya anasema mapinduzi hayo ndiyo kwanza yameanza.

“Baadaye itakuwa zaidi ya hapa, mikutano mingi ya siasa itakuwa ´live´ Facebook au Instagram au Youtube, huu ni mwanzo tu. Mapinduzi halisi bado.

No comments:

Theme images by merrymoonmary. Powered by Blogger.