Header Ads

ad

RAIS MAGUFULI NA RAIS MUSEVENI WAMEWEKA JIWE LA MSINGI LA MRADI WA BOMBA LA MAFUTA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni wameweka jiwe la msingi la Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki ( EACOP) katika kijiji cha Luzinga, Mutukula nchini Uganda.

Sherehe za kuweka jiwe la msingi la mradi huo zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais wa Uganda Mhe. Edward Kiwanuka Sekandi, Mke wa Rais Magufuli Mhe. Mama Janeth Magufuli, Mke wa Rais Museven Mhe. Mama Janeth Museveni, Naibu Waziri Mkuu wa 3 wa Uganda Mhe. Kirunda Kivenjinja, Mawaziri wa Tanzania na Uganda, viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama na viongozi wa taasisi mbalimbali za nchi zote mbili.

Upande wa Tanzania sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi la mradi huu zilifanyika tarehe 05 Agosti, 2017 katika Kijiji cha Chongoleani Mkoani Tanga.
Bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki litaanzia Wilaya ya Hoima nchini Uganda ambako kumegunduliwa kuwepo kwa mafuta ghafi mapipa Bilioni 6.5 ambayo yatasafirishwa kwa bomba kwa kiasi cha mapipa 216,000 kila siku hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania ambako yatakwenda katika masoko mbalimbali duniani.

Bomba hili litakuwa na urefu wa kilometa 1,445 ambapo kati yake kilometa 1,149 zitapita katika Mikoa 8 na Wilaya 24 za Tanzania, na wakati wa ujenzi mradi huu unatarajiwa kutoa ajira kwa watu 10,000.

Bomba hili litajengwa na kuendeshwa na Kampuni ya Bomba la Mafuta kwa ubia na Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda (NOC), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na kampuni tatu za mafuta za CNOOC, TOTAL na TULLOW kwa gharama ya Dola za Marekani Bilioni 3.5.

Akizungumza katika sherehe hizo Mhe. Rais Magufuli amemshukuru na kumpongeza Mhe. Rais Museveni kwa kufanikisha ugunduzi wa mafuta na kukubali bomba la kuyasafirisha kupitia Tanzania, na amemhakikishia kuwa Tanzania itatoa ushirikiano wa kutosha wakati wa ujenzi na uendeshaji wake.

“Mhe. Rais Museveni kwa kutekeleza mradi huu umeleta ustawi wa wananchi wa Uganda na pia umeleta ustawi wa wananchi wa Tanzania, mradi huu utaleta manufaa makubwa ya kiuchumi kwa nchi zetu na watu wetu, napenda kukushukuru sana wewe, wawekezaji wanaokuja kujenga bomba hili na wote walioshiriki kuufikisha mradi huu hapa, pia naomba wale vijana wa Uganda waliogundua mafuta uwape tuzo ya kutambua mchango wao na kulijengea heshima Bara la Afrika, kuwa nasi tunaweza kugundua mafuta” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Kwa upande wake Mhe. Rais Museveni ameelezea kufurahishwa kwake na mradi huo na amesema ana matumaini kuwa utaleta manufaa makubwa kwa nchi zote mbili.
Mapema kabla ya kuweka jiwe la msingi la mradi huo Mhe. Rais Magufuli amepokelewa rasmi na mwenyeji wake Mhe. Rais Museveni aliyemwalika kwa ziara rasmi ya kiserikali ya siku 3, na baadaye viongozi hao wawili wamezindua kituo cha pamoja cha huduma za mpakani ( One Stop Border Post – OSBP ) kilichopo Mutukula.
Kituo hiki kilianza kujengwa mwaka 2011 na kuanza kutoa huduma mwaka 2015 na kimesaidia kuharakisha utoaji wa huduma za mpaka kulikowezesha kukua kwa ukusanyaji wa mapato, kuokoa muda na kukuza biashara kati ya Tanzania na Uganda.
Kituo hicho kimejengwa na Tanzania na Uganda kwa ufadhili kutoka asasi ya Trade Mark East Africa na kugharimu Shilingi Bilioni 7.3

Mhe. Rais Magufuli na Mhe. Rais Museveni wamefanya mkutano wa hadhara katika Wilaya ya Kyotera nchini Uganda na kuwasisitiza wananchi wa Tanzania na Uganda kutumia uhusiano na ushirikiano mzuri na wakidugu uliopo kati ya nchi hizi, kujenga uchumi kwa kasi zaidi kwa kufanya biashara pamoja na kuzitumia ipasavyo fursa mbalimbali ikiwemo kituo cha pamoja cha huduma za mpakani na bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki ambalo litatoa ajira na kuwezesha biashara na shughuli mbalimbali zitakazoambatana na ujenzi wa bomba hilo.

“Naomba niwahakikishie wananchi wa Uganda, nyinyi ni ndugu zetu na sisi Tanzania tupo pamoja na nyinyi, tumezindua kituo cha pamoja cha huduma za mpakani na tumeweka jiwe la msingi ujenzi wa bomba la mafuta, naomba mchangamke, fanyeni biashara, wananchi wa Uganda nendeni Tanzania na Watanzania watakuja huku Uganda, hayo ndio manufaa ya uhusiano na undugu wetu” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Kyotera, Uganda
09 Novemba, 2017

No comments:

Theme images by merrymoonmary. Powered by Blogger.