Header Ads

ad

DALILI HIZI ZINAONYESHA KAMA UNAWEZA KUSIMAMIA FEDHA ZAKO AU LA

Katika maisha ya kila siku watu hufanya kila namna ili kujipatia fedha za kuwawezesha kuishi maisha wayatakayo. Watu wengi hasa wafanyakazi walioajiriwa na kutegemea malipo ya mshahara mwisho wa mwezi, hujiwekea mipango ya namna ya
kuitumia fesha yao kwa umakini.
Wengi hupanga bajeti na kuhakikisha kuwa wanabaki na akiba kiasi ambayo itawawezesha kufanya vitu vya dharura ambavyo huwezi kuvipanga. Mfano ugonjwa, msiba na matukio mengine kama hayo.

Ni vizuri kujiwekea akiba ya fedha katika maisha yako kwani akiba hiyo inaweza kukusaidia wakati unapokumbana na hali ngumu.
Unadhani utaishi vipi pale umeenda kazini na kukuta barua ya kusimamishwa kazi? Kama hukuwa umejiwekea akiba utakumbana na hali ngumu ya maisha mpaka pale utakapopata kazi nyinine. Je! Itakuwaje kama usipopata kazi nyingine?\

Umeuona sasa umihimu wa kujiwekea akiba katika maisha? Huo ni mfano mdogo tu. Zipo hali nyingine kubwa zinazoweza kukupata na kama hukuwa umejiwekea akiba ukaishia kupata matatizo makubwa.

Wapo watu wengi wanaopata fedha nyingi katika Maisha yao lakini hawawi na mafanikio makubwa kwa sababu ya tabia zao za kutumia hovyo kipato chao.
Baadhi wanapopokea mshahara wanawaalika rafiki zao kwenda baa kunywa pombe na kustarehe. Ama mtu ananunua vitu vya gharama na visivyo vya msingi kwa kutumia fedha nyingi. Mfano kununua nguo nyingi za gharama kubwa, kwenda maeneo ya starehe na tabia zingine zinazofanana na hizo.

Hapa chini tumeonyesha baadhi ya mambo ambayo kama umekuwa ukiyafanya ama yanakukumba, basi unahitaji msaada mkubwa wa usimamizi katika matumizi ya fedha zako.
Kuchelewesha malipo

Imefika mwisho wa mwezi, lakini bado hata hujajua utakapopata kodi ya nyumba, ankara ya maji nayo inaletwa lakini huna fedha ya kuilipa. Hujakaa vizuri LUKU nayo inaisha unalala gizani kwa kukosa fedha ya kununua umeme. Haya ni baadhi tu ya matatizo yanayowakumba watu wanaotumia fedha pasipo utaratibu maalum.

Hali hii kama imewahi kukukumba ama ndiyo unapambana nayo basi unahitaji msaada wa uangalizi wa fedha zako.
Tabia ya kutoa fedha benki mara kwa mara.
Watu wenye matumizi mazuri ya pesa hupanga bajeti yao ya muda mrefu ili kuepusha matumizi yasiyo ya lazima. Kuna wakati dharura hutokea na inakulazimu kwenda benki kutoa fedha. Lakini kama una kawaida ya kwenda kutoa fedha zako ulizoziweka kama akiba benki mara kwa mara, basi ujue una matumizi mabaya ya fedha na unahitaji usimamizi wa hali ya juu katika kutumia pesa ulizonazo.

Kukopa mikopo kwa matumizi yasiyo ya msingi
Kukopa siyo jambo baya katika Maisha, lakini inabidi ujue unakopa kwa lengo gani. Ukikopa kwa lengo la kulipa gharama za matibabu yako ni sahihi, lakini unapokopa kiasi kikubwa cha fedha kwa lengo la kwenda mapumziko au kwenda kufanya starehe, hapo unahitaji kupata msaada wa karibu wa namna ya kuzitunza fedha zako.

Unapokuwa na madeni mengi kuliko uwezo wako.
Pale unapokuwa mtu wa matumizi yasiyo na msingi kama vile kwenda sehemu za starehe ambazo unatumia fedha nyingi bila kuingiza kipato chochote, utaishia kuwa mkopaji kwa kuwa utaishiwa na fedha kila mara. Hapo ndipo utakapojikuta katika wimbi la madeni ambayo hutoweza kuyalipa kwa wakati au ukashindwa kulipa kabisa na mwisho wa siku kuishia gerezani.
Unaweza kupambana na hali hii kwa kufanya kazi kwa bidi na kuhakikisha kuwa unapunguza kama siyo kuondoa kabisa tabia ya kutumia fedha katika mambo yasiyo ya msingi.
Theme images by merrymoonmary. Powered by Blogger.