Simba yatuma salamu kwa Yanga
Klabu ya soka ya Simba imeendelea kuongoza msimamo wa ligi kuu soka Tanzania Bara baada ya kufanikiwa kuiadhibu Njombe Mji mabao 4-0 kwenye mchezo wa raundi ya 7 uliomalizika jioni hii kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.
Katika mchezo huo Simba ilianza kwa kushambulia lakini Njombe Mji walijitahidi kuwadhibiti washambuliaji wa Simba hadi dakika ya 28 ambapo mshambuliaji Emmanuel Okwi alifanikiwa kuiandikia Simba bao la kuongoza ambalo lilidumu hadi mapumziko.
Kipindi cha pili Simba walirejea kwa kasi na kuliandama lango la Njombe Mji ambapo katika dakika ya 51, kiungo Mzamiru Yassin alifanikiwa kufunga bao la pili kabla ya kuongeza bao la tatu dakika ya 52. Simba iliendelea kushambulia na kufunga bao la nne kupitia kwa Laudit Mavugo.
Simba sasa inaongoza ligi ikiwa na alama 15 sawa na Mtibwa Sugar ambayo nayo imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons. Azam FC imetoka sare ya 0-0 na Mbao FC wakati Lipuli FC imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Majimaji FC. Matokeo mengine Ndanda FC imetoka sare ya 0-0 dhidi ya Singida United.
Emmanuel Okwi sasa amefikisha mabao 8 akiwa anaongoza orodha ya wafungaji msimu huu. Baada ya mchezo wa leo Simba itaelekea visiwani Zanzibar kujiwinda na mchezo dhidi ya watani wao wa jadi Yanga wikiendi ijayo.
No comments: