Lijualikali Ajisalimisha Polisi Morogoro
Walifikishwa kituoni hapo Jumanne Novemba 28,2017 baada ya kukamatwa Jumapili Novemba 26,2017 saa tano usiku wakituhumiwa kufanya fujo zilizohusisha uharibifu wa mali za umma.
Vurugu hizo zilitokea baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kata ya Sofi wakituhumiwa kuchoma moto ofisi za taasisi za umma yakiwemo majengo ya shule ya msingi Sofi, ofisi ya mtendaji kata na nyumba ya walimu wa shule hiyo.
Lijualikali ambaye polisi ilisema naye anahusishwa na vurugu hizo, amejisalimisha polisi leo Alhamisi Novemba 30,2017 saa nne asubuhi. Katika kituo hicho cha polisi ulinzi umeimarishwa.
Gari aina ya Pick -up mali ya Chadema ndilo lililompeleka Lijualikali kituoni hapo na kabla ya kukaribia lango kuu la kituo hicho, askari alilizuia kuingia ndani.
Mbunge huyo baada ya kushuka ndani ya gari askari walimsindikiza kuingia kituoni huku wakiwazuia wananchi kulikaribia lango kuu la kituo hicho.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Urlich Matei katika taarifa Jumatatu Novemba 27,2017 alisema wanaendelea kuwatafuta watu wengine waliohusika na vurugu hizo, akiwemo mbunge Lijualikali.
Mbunge Lijualikali akizungumza na MCL Digital kwa simu kuhusu vurugu hizo alisema wakati matokeo yakitangazwa alikuwa Ifakara.
Alisema taarifa za kutafutwa na polisi ndiyo kwanza alizisikia kutoka kwa mwandishi wa habari wa MCL Digital.
“Baada ya kumalizika kampeni Jumamosi nilirejea Ifakara kwa hiyo sijui chochote kuhusu hizo vurugu na nashangazwa kuhusishwa na tuhuma hizo, lakini kama kweli natafutwa nitakwenda kujisalimisha polisi,” amesema Lijualikali.
No comments: