Header Ads

ad

BUNGE LACHUKUA MAAMUZI HAYA MAGUMU SAKATA LA MAFUTA YA KULA

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, ameitaka serikali kusema ukweli na kuacha ubabaishaji kuhusu suala la mafuta ya kula kwani wananchi ndio wanaoumia.

Spika Ndugai ameyasema hayo leo mchana wakati akiongoza kikao cha Bunge ambapo Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alikuwa akitoa maelezo kuhusu hali ya mafuta ya kula ambayo yameanza kuadimika mitaa na kupanda bei, kutokana na meli zenye mafuta ya kula kukwama bandarini kwa zaidi ya wiki mbili sasa.

Akitoa maelezo ya serikali, Waziri Mwijage alisema kuwa, kukwama huko kwa meli kumetokana na kupishana kwa ripoti ya Wakala wa Vipimo Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhusu aina ya mafuta yaliyomo kwenye meli hiyo.

Waziri Mwijage amesema kuwa, TBS wameonesha kwamba mafuta hayo ni ghafi lakini TRA wamekataa na kusema kwamba yamechakatwa kiasi (semi-refined) na hivyo mkanganyiko huo unapelekea mzigo kushindwa kutolewa kutokana na kwamba haijulikani ni kiasi gani cha kodi kitatozwa.

Kufuatia hali hiyo, Spika Ndugai amesema bungeni hakuwezi kukawa ni sehemu ya kusemewa uongo na kwamba mambo yakienda hivyo hatuwezi kufika.
Kufuatia hali hiyo, alimtaka Waziri Mwijage atakaporudi bungeni kwenye kikao cha jioni leo saa 11, awe na majibu ya uhakika kuhusu sakata la mafuta ya kula kwani wananchi ndio wanaoumia.

Spika Ndugai ameonesha kushangazwa na jambo dogo la upimaji wa mafuta kuchukua muda mrefu, na kusema kwamba, kama TRA hawaamini wakemia wa TBS basi sampuli ya mafuta yachukuliwe yapelekwe Afrika Kusini kwa ajili ya kupimwa ili mzigo huo uondolewe bandarini.

“Mnatufikisha mahali pagumu sana, kwa mambo madogo sana. Hivi kweli nchii leo, wale wote tuliosoma Chemistry pamoja na mimi, hivi kweli kupima mafuta kujua kama ni semi-refined au ni crude, hiyo kweli ni rocket science?” amehoji Spika.

Amesema hapo hakuna ubishi na kwamba haiwezekani mbabe mmoja (TRA) akakwamisha mambo. Asisitiza mafuta hayo yatozwe kodi stahiki yaingie sokoni kwani yanavyozidi kukaa bandarini, wanaoumia ni wananchi na wao ndio watakaolipa gharama zote zinazotokana na ucheleweshwa huo.

No comments:

Theme images by merrymoonmary. Powered by Blogger.